
Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametishia kuwafunga jela kwa miaka 10 watu watakaomtukana au kumdhalilisha Rais Yoweri Museveni, mwanafamilia wa Museveni ikiwemo yeye mwenyewe.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, Muhoozi, ambaye pia ni mwanaye Rais Museveni, alitoa onyo jingine kwa mashirika ya habari ya kimataifa yanayofanya kazi nchini Uganda, akidokeza kuwa serikali inapanga kuanzisha sera mpya itakayosimamia jinsi wanaendesha shughuli zao.
“Karibuni nitatangaza sera mpya kuhusu shughuli za vyombo vyote vya habari vya kigeni nchini Uganda. Siku zao za kuitukana nchi yetu zimefika mwisho,” aliandika Muhoozi.
Hata hivyo, bado hajaeleza kwa kina sera hiyo inayopendekezwa wala kutaja hatua ambazo vyombo vya habari vya kigeni vinaweza kuchukuliwa.
Vitisho hivyo vinatolewa takriban siku kumi baada ya shirika la habari la AFP kuripoti, likinukuu vyanzo ndani ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), kuwa maafisa wakuu wa chama hicho walikuwa wamekataa pendekezo la Rais Museveni la kumtaka mwanawe kuwa mrithi wake.
Hata hivyo, NRM imekanusha taarifa hizo.
Licha ya katiba ya Uganda pamoja na kanuni za maadili za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kuwataka maafisa wa kijeshi kutokuwa na misimamoya kisiasa na kuwazuia kushiriki katika shughuli za kisiasa za vyama, Muhoozi amekuwa akieleza mara kwa mara nia yake ya kuwania urais na kutoa vitisho dhidi ya viongozi wa upinzani.
