
Jeshi la Iran limesema limedungua ndege isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-1 katika eneo la Kohistakh.
Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, limeripoti kuwa ndege hiyo ilidunguliwa kufuatia kile lilichokitaja kuwa ni operesheni iliyofanikiwa ya kuizuia na kuishambulia kwa kutumia mfumo mpya wa ulinzi wa anga wa jeshi la wanamaji.
IRNA pia lilichapisha picha lilizodai kuwa zinaonesha mabaki ya ndege hiyo baada ya kudunguliwa.
Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) haijatoa majibu kuhusu madai hayo ya Iran.
Katika taarifa tofauti, CENTCOM imesema Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) lilirusha ndege mbili zisizo na rubani zilizotengenezwa kwa ajili ya mashambulizi ya kujitoa mhanga kuelekea Bahrain, lakini vikosi vya Marekani vilifanikiwa kuzidungua kabla hazijafika zilipokuwa zikielekea.
CENTCOM imeongeza kuwa tukio hilo halikusababisha vifo, majeruhi wala uharibifu wa mali.
Kwa upande wake, Walinzi wa Mapinduzi ya Iran wamesema walilenga na kuharibu rada ya Marekani inayotumika kutoa tahadhari za mapema kuhusu mashambulizi ya kijeshi, iliyoko Bahrain, katika shambulizi lililotokea Ijumaa asubuhi.
Katika taarifa yao, wamesema shambulizi hilo lilikuwa ni kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi la anga la Marekani lililofanyika katika eneo la Sirek usiku uliotangulia.
Walinzi hao wa Mapinduzi wametoa onyo kwa Marekani, wakitaka isimamishe kile walichokitaja kuwa ni vitendo vya uchokozi angani pamoja na magendo ya mafuta katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Aidha, wameonya kuwa iwapo Marekani itaendelea na kile walichokitaja kuwa ukiukaji na uchokozi, vikosi vya anga na anga za juu vya Iran vitawekwa katika hali ya tahadhari ya juu kwa ajili ya kile walichokiita makabiliano yasiyo na mipaka.
