
Chama tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM), kimepinga pendekezo la kumtaka Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe Rais Yoweri Museveni, kuwa mrithi wake wa kisiasa, hatua inayoashiria kuwepo kwa upinzani ndani ya chama hicho dhidi ya uwezekano wa mamlaka kukabidhiwa kutoka kwa baba kwenda kwa mwanawe.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, watu watano waliohudhuria mkutano wa faragha wa kamati kuu ya utendaji ya NRM wamesema baadhi ya wajumbe walipinga azma ya Kainerugaba kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2031.
Katika mkutano huo uliofanyika Jumanne na kuitishwa kujadili suala la urithi wa uongozi wa Rais Museveni, wajumbe walijadili uwezekano wa kumpitisha mkuu huyo wa jeshi kama mgombea wa chama hicho.
Hata hivyo, kura iliyokuwa imepangwa kuhusu ugombea wake ilisitishwa baada ya wajumbe kadhaa kati ya 28 wa kamati hiyo kuzungumza kupinga pendekezo hilo, huku wakipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wengine.
Vyanzo hivyo vimesema wajumbe wanne walikuwa wamepiga kura kumuunga mkono Kainerugaba, huku watatu wakimpinga, kabla zoezi hilo halijasitishwa.
Rais Museveni mwenye umri wa miaka 82 ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986. Mwanawe Muhoozi, mwenye umri wa miaka 52, kwa sasa ndiye mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na amekuwa akijitokeza zaidi katika siasa za Uganda huku mjadala kuhusu atakayemrithi rais huyo ukizidi kushika kasi.
Kainerugaba ametangaza nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2031. Hata hivyo, matarajio yake ya kisiasa yameibua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wanachama wa chama tawala, hasa kutokana na mwenendo wake na jumbe zenye utata ambazo amekuwa akichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Chanzo kimoja ndani ya chama hicho kimeiambia AFP kuwa mtindo wake wa kukabiliana na watu kwa ukali umesababisha baadhi ya wanachama kutokuwa na amani kuhusu uongozi wake.
Chanzo kingine kimesema Rais Museveni ameshauriwa kumuondoa mwanawe jeshini na kumpa wadhifa wa kiraia ili aweze kuelewa vyema wananchi na kujiandaa kwa majukumu ya uongozi.
Rais Museveni aliibua kwa mara ya kwanza suala la urithi wa uongozi mwishoni mwa mwezi Oktoba alipokutana na viongozi wakuu wa chama hicho.
Katika mkutano huo, aliwasilisha waraka ambao ndani yake alieleza kuwa mwanawe ana sifa zinazohitajika kuiongoza Uganda.
