
Mwalimu wa zamani nchini Australia amehukumiwa kifungo cha miaka minane na miezi sita jela baada ya kumnyanyasa kingono mvulana aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati unyanyasaji huo ulipoanza na baadaye kumzaa mtoto wake.
Naomi Tekea Craig, mwenye umri wa miaka 34, alikiri makosa 12 ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto huko Magharibi mwa Australia.
Mahakama ilisikia kwamba Craig alikutana na mvulana huyo alipokuwa akifanya kazi kama mwalimu wa muziki katika shule yake huko Mandurah, kusini mwa Perth, mwaka wa 2023.
Baadaye alijenga uhusiano wa karibu na familia yake, akawa rafiki na mama yake na kusaidia mara kwa mara na usafiri wa shule.
Licha ya mvulana huyo kuhamia shule nyingine, Craig aliendelea kutumia muda pamoja naye na hatimaye akapewa ufunguo wa nyumba ya familia hiyo.
Unyanyasaji huo ulianza wakati mvulana huyo akiwa na umri wa miaka 12 na uliendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Vitendo hivyo viligundulika baada ya mama wa mvulana huyo kupata mashaka na kuweka kamera za usalama ndani ya nyumba ya familia. Picha kutoka kwenye kamera hizo zilikabidhiwa kwa polisi.
Craig alikamatwa mnamo Desemba 2025 na akajifungua mtoto wa kike mwezi uliofuata. Vipimo vya vinasaba (DNA) vilithibitisha kuwa mvulana huyo ndiye baba wa mtoto huyo.
Wakati wa kutoa hukumu katika Mahakama ya Wilaya ya Perth mnamo tarehe 17 Novemba 2026, Jaji John Prior alielezea vitendo vya Craig kama ukiukaji mkubwa wa imani.
Mahakama ilielezwa kuwa Craig alikuwa akimnunulia mvulana huyo zawadi, akifuatilia shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii, na kumwambia kuwa anataka kupata watoto zaidi naye.
Waendesha mashtaka walisema kuwa unyanyasaji huo una uwezekano wa kuacha madhara ya kudumu kwa mvulana huyo na familia yake.
Craig atakuwa na sifa za kuomba kuachiwa kwa masharti (parole) baada ya kutumikia kifungo cha miaka sita na miezi sita.
Utambulisho wa mvulana huyo hauwezi kuwekwa wazi kwa sababu za kisheria na kwa ajili ya usalama wake
