
Jeshi la Uganda (UPDF) limetangaza kuwa litawaondoa wanajeshi wake katika mji wa Lubero, ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ndani ya wiki mbili zijazo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Uganda, usalama wa mji huo utakabidhiwa kwa jeshi la Congo (FARDC) baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa Uganda.
UPDF imekuwa ikifanya operesheni katika eneo hilo tangu mwezi Januari 2025, katika juhudi za kuwadhibiti wapiganaji wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) waliokuwa wakitoroka mashambulizi ya pamoja ya kijeshi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Kanali Chris Magezi, Kaimu Mkurugenzi wa Habari katika jeshi la UPDF, haikufafanua sababu za uamuzi wa kuwaondoa wanajeshi hao kutoka Lubero.
Aidha hapo jana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilimwita balozi wa Uganda mjini Kinshasa kufafanua machapisho ya mitandao ya kijamii ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa rais wa nchi hiyo.
Katika mfululizo wa machapisho kwenye mtandao wa X, Jenerali Kainerugaba alisema kuna uwezekano wa waasi kuiteka mji wa Walikale, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DR Congo.
Uganda na DRC zilianzisha operesheni ya pamoja ya kijeshi mwezi Novemba 2021 dhidi ya ADF na makundi mengine yenye silaha katika eneo hilo, kwa lengo la kudhoofisha na kuangamiza uwezo wao wa kuhatarisha usalama wa eneo hilo
