Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) imemwita mwanadiplomasia mkuu wa Uganda mjini Kinshasa kufuatia machapisho ya mitandao ya kijamii ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwana wa rais wa nchi hiyo.
Katika mfululizo wa machapisho kwenye mtandao wa X, Jenerali Kainerugaba alionekana kuunga mkono uwezekano wa waasi kuiteka Walikale, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DR Congo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa uwepo wa jeshi la Uganda nchini humo unalenga masuala ya usalama pekee.
Wizara ya Mambo ya Nje ya DR Congo ilimwita balozi wa Uganda kueleza matamshi hayo, ikiyataja kuwa “ya hatari sana” na yanayoweza kuathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Serikali ya Uganda haikuwa imetoa majibu yoyote kufikia sasa.
Mvutano huu wa kidiplomasia umeibuka licha ya ushirikiano wa karibu wa kijeshi kati ya nchi hizo jirani.
Tangu mwaka 2021, majeshi ya Uganda na DR Congo yamekuwa yakifanya operesheni za pamoja dhidi ya kundi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye uhusiano na kundi la Islamic State, mashariki mwa DR Congo.
Uganda pia imekuwa ikihusika katika juhudi za upatanishi kati ya serikali ya Congo na kundi lenye silaha linaloongozwa na aliyekuwa mbabe wa vita, Thomas Lubanga, katika jimbo la Ituri.
Katika machapisho yake, Jenerali Kainerugaba aliishutumu Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi lenye silaha linalofanya shughuli zake mashariki mwa DR Congo, kwa kuwalenga watu wa jamii ya Bahima.
Wabahema ni jamii ya wafugaji wa jadi inayopatikana zaidi katika jimbo la Ituri kaskazini mashariki mwa DR Congo. Jamii hiyo ina uhusiano wa kihistoria na kitamaduni na Wabahima wa Uganda.
Jenerali huyo pia alitoa vitisho vya kuungwa mkono kwa utekaji wa Walikale na waasi, huku akitetea uwepo wa jeshi la Uganda nchini DR Congo.
Walikale ni eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, likiwemo baadhi ya machimbo makubwa ya bati na dhahabu nchini humo.
Akaunti ya X ya Jenerali Kainerugaba, iliyokuwa na karibu wafuasi milioni 1.4, baadaye haikuweza kupatikana.
Haijulikani iwapo aliifunga mwenyewe kama alivyowahi kufanya hapo awali au kama jukwaa hilo liliisimamisha.
Katika wiki hiyo hiyo, alitangaza:
“Machapisho yangu kwenye X nchini Uganda ni maagizo ambayo lazima yatekelezwe.”
