Na Sam Ruhuza
Askofu Gwajima aliita press conference kama Mtanzania na kuongelea suala la Utekaji na kulaani pakubwa watekaji na kuonyesha kuumia sana na hali hiyo hadi kuwatolea mfano watoto wa wakuu akiwamo mkuu kabisa, akihoji iwapo wangevumilia watu wasiojulikana kuendelea kuteka?!
Kilichofuata baada ya kauli yake;
– Wabunge wenzake wa chama chake, badala ya kujadili bajeti ya Wizara ya Ndani, wao wakaishia kumjadili Gwajima na kulaani mfano wake wa kuteka mtoto wa Mkuu! Wengine tuliona ujumbe umefika maana waliumia na ndio ilikuwa nia ya mfano huo, zaidi ya maneno yao ilikuwa uchawa tu majina yao yapitishwe kwenye uchaguzi ndani ya chama!!
– Mkiti wa chama chake kwenye mkutano mkuu aliwataka wanachama kuwaacha wakina Gwajima, yaani wenye mawazo kama ya Gwajima na kuwaita Gwajimanized chama!
– Ubunge wake ndipo ulipoishia hapo!
– Alipotangaza kufunga na kusali kwa Makanisa anayoyaongoza kwa ajili ya kuliombea Taifa lipone dhidi ya Utekaji, kesho yake Kanisa yaani Dhehebu lake nchi nzima likafutwa kwa Msajili!
– Tukaanza kuona kwenye videos Waumini wa Kanisa lake wakaanza kushambuliwa kwa marungu na Police kila walipokwenda Kanisani kuabudu!
Hadi leo hatujasikia Kanisa au Dhehebu hilo likifunguliwa!!
Naendelea kuwaza kwa sauti, leo chama cha siasa chadema tumewasikia wakienda kufariji familia za waliotekwa na wengine kuamua kwenda Kanisani kuabudu na kumuomba Mungu, inaelezwa Police wamewavamia Kanisani wakiwa kwenye sala na kuwachukua!!!
Nawaza kwa sauti huku nikikosa majibu, kwanini anayeongelea au kuombea utekaji ukome, anapata mtihani na Police, Kulikoni?!
Kwanini haya yanatokea Kanisani kwenye Ibada?!
Ninawaza, Je ni majibu ya Mungu kuonyesha watekaji?!
Kwanini Wabunge walimlaani sana Mbunge mwenzao Gwajima kwa hoja yake badala ya angalau kujadiliana Utekaji, mbona Mheshimiwa Rais alipoongelea kutopendezewa na hali ya Utekaji na kuwataka Police kuchukua hatua, haohao Wabunge walishangalia, nini tofauti yake??!!
Nawaza kwa sauti, chama tawala kilipoambiwa kujitenga na wakina Gwajima na wajumbe kushangilia, walielewa nini??!! Au Mkiti wao alimaanisha nini??!!
Je, kwa Mwananchi kuongelea Utekaji au kumuomba Mungu akomeshe hili ni kosa la jinai?! Inabidi tuambiwe ili tuelewe!
Je, Chadema kuwa na matukio mengi ya kukamatwa kamatwa makosa yao ni nini ili tuelewe, labda mtu kuwa chadema ni makosa?!
Nawaza kwa sauti mfumo wa vyama vingi vya siasa ulivyoanza na kuendelea, japo ulikuwa mgeni na mapungufu yalikuwapo, lakini watu waliongea na kufurahi pamoja, hii watu wasiojulikana walipoanza kazi zao, hali imekuwa sio sawa, ni kuogopana na kuhisi mmoja ana haki zaidi ya mwingine!

Taifa linapona kwa mijadala.
Muhimu Tupendane na kuheshimu mawazo ya mwingine hata kama huyapendi!
Tanzania ni yetu sote! 


