Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliye nijalia kwa rehma zake mfungo wa Ramadhan salama salimin. ALHAMDULILLAH.
Hoja yangu ya leo ni UAMSHO kwa ndugu zangu waafrika juu ya nadharia ya Uchumi kuwa NI elimu ya juu ya mfumo bora wa maendeleo ya watu na nchi zote duniani. Mfumo mmoja kandamizi kwa wote. Labda nusjereheshe hapa chini..
Hoja yangu inahusu Elimu hii ya Uchumi ambayo kwanza inatudhalilisha sana sisi Waafrika kama kwamba sisi hatuwezi kufikiri nje ya mfumo huo isipokuwa kwa mapokezi ya mafundisho ya Wakoloni walotutawala na wakafaidika na rasilimali zetu kwa njia za udanganyifu wa mapambo ya wadhifa ya Uhuru wa bendera.
Hivi leo tunapodai tupo huru, uhuru huo tunao kweli ikiwa bado tunatumia Elimu ya Uchumi wa Ukoloni Mambo leo? Tofauti gani iliyopo na Ukoloni ule ikiwa leo wakoloni wanakuja nchini kama wawekezaji wakiwa na matrillioni ya fedha walizo zichapisha wao wenyewe toka viwanda vyao, na kutuhadaa kwa mikataba walioandika wao, kisha wakachimba na kuchukua dhahabu yetu, wakaichua na kuiweka katika hazina zao kwa thamanisho sawa na karatasi walizochapisha wao zikithaminishwa kama ni fedha?
Hivi kweli sisi Waafrika kwa akili gani tulizojaaliwa, tunakubali kuhodhi kama akiba yetu hazina hizo karatasi ambazo hazina thamani ila kwa mzani wa Wakoloni wakati wao wamehifadhi dhahabu yetu kwa gharama ya karatasi walizochapisha kama fedha! Sijui kama nimeeleweka hapo..
Yawezeka mimi nashindwa kuelewa mantiki ya Biashara hii mnijuze wataalam wa Uchumi. Inawezekanaje kampuni ya madini kutoka Marekani, Canada, Uingereza au Australia inawekeza mathlan dollar millioni 300 ambazo watanunua vifaa vinavyotegenezwa kwao wenyewe kuja kuchimba dhahabu ilihali mzunguko wa fedha hizo za uwekezaji umebakia kwao? (Mtaji wa uwekezaji ni karatasi zao na wamenunua zana zao) kuja kuchimba madini yetu kwa ahadi ya faida ya mauzo yao sii yetu!
Kampuni zao za utengenezaji zana na uchimbaji ndizo zIlofaidika na matrillioni ya fedha hizo kukuza Uchumi wao wa ndani, halafu wanakuja kwetu wanachimba dhahabu kama mali yao na kuondoka nazo kwa faida nyingine wakati sisi tunaachiwa mashimo yalojaa kemikali hatariahi kwa mazingira yetu wakitupa matumaini ya kuvuna karatasi walochapisha wao kama fedha na akiba yetu.
Kwa maana nyingine tumenufaika na karatasi zao na kuzilimbikiza hazina kama pato la Taifa lakini lenye deni kubwa zaidi kwa sababu tulikopa fedha nyingine kutoka kwao zenye riba ili kutengeneza barabara, nguvu ya umeme, maji, mawasiliano na kadhalika. Kibindoni hazina tumeshehena karatasi ambazo tunajigamba kuwa na uchumi imara na tuna akiba ya kutosha.
Mimi naamini hapa hakuna usawa kabisa na inatakiwa Hatua ya Uthibitisho (affirmative action) juu ya dhulma hii ambayo imetulemaza nchi maskini na kubakia tegemezi miaka yote.
Huu ni wakati muafaka kwa Waafrika tuamke ili haki itendeke maana tusipoweza kutambua ghirba hii ya Elimu ya Uchumi na maendeleo basi tutaendelea kujenga maghorofa kama mahekalu ya Pyramid ilihali maisha ya Wananchi yataendelea kuwa duni kwa sababu hawa wakoloni wana hila na katu hawaweza kutupa elimu yenye manufaa kwetu. Haiwezekani wao wahifadhi dhahabu yetu kama akiba ya utajiri wao, wakati sisi tumeshehena karatasi zao hazina.
Allahu yaalam, sijui ni lini lakini itafika wakati sisi tutazitafuta hizo dhahabu tusiwe nazo tena, halafu itatulazimu sisi tuzinunue kutoka kwao kwa gharama nyingine kabisa wala sii tena karatasi zao bali Uhai wetu.
Uamsho – Akutendae mtende, mche asiyekutenda.
Maasalaam – EID MUBARAK